POLISI AUWA KWA NONDO MKOANI MBEYA

Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya advocate nyombI
JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya limekiri kushindwa kuwadhibiti wahalifu wa upigaji nondo ambao jana walimuua askari mwenye namba G.2795 Konstebo Meshack (28).
Kuuawa kwa askari polisi huyo maeneo ya Mabatini kulifuatiwa tukio jingine kama hilo ambapo askari wa usalama barabarani aliyefahamika kwa jina la Hawa ambaye sasa yuko mahututi na amelazwa katika hospitali ya Rufaa ya Mbeya baada ya kupigwa nondo maeneo ya Meta.
Kabla ya askari polisi hao kupigwa nondo na mmoja kuuawa, tukio la kwanza la upigaji nondo na kushambulia mwilini alipigwa askari Flora aliyepigwa maeneo ya Uyole ambapo katika tukio hilo, Richard Shitambala aliuawa.
Katika mfululizo wa matukio hayo wameumizwa wananchi zaidi ya 20 kwa kipindi cha miezi miwili ambapo katika tukio la jana pekee watu tisa walifikishwa katika hospitali ya rufaa ya Mbeya wakiwa wamejeruhiwa vibaya.
Akizungumza na waandishi wa habari hospitalini hapo jana, mganga wa idara ya wagonjwa wa nje na huduma ya haraka, Dk. Dominic Chalu, alisema majeruhi tisa walifikishwa usiku wa kuamkia jana ambapo majeruhi wanne waliruhusiwa kurudi nyumbani.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na Tanzania Daima Jumatano waliofika kuwaona majeruhi hospitalini hapo walisema Jeshi la Polisi mkoani hapa linapaswa kujipanga na kuondoa mlundikano wa trafiki barabarani badala yake waimarishe doria za wahalifu wakiwemo wapiga nondo.
Wakati huohuo, kota ya askari polisi wa kituo kikuu cha polisi mkoani hapa imeungua moto na kuteketeza baadhi ya vitu vilivyokuwemo ndani ya nyumba hiyo.
Tukio hilo lililotokea juzi lilishuhudiwa na Tanzania Daima na moto huo kuzimwa na wananchi waliokuwa wakinywa pombe katika kantini ya jeshi hilo.
SOURCE;TANZANIA DAIMA.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya Advocate Nyombi amesema kuwa askari huyo amesafirishwa jana wenda nyumbani kwao mkoani Arusha mara baada ya taratibu kukamilika.

Comments
Post a Comment